Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Emmerson Mnangangwa amesema serikali yake itaendelea kushirikiana na kuimarisha uhusiano wake na Tanzania ili kuimarisha uchumi wa nchi hizo mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es salaam leo, Rais Mnangagwa amesema kuwa Tanzania imesaidia kwa kiasi kikubwa katika harakati za ukombozi wa nchi za Zimbabwe, Afrika Kusini, Namibia na Msumbiji na hivyo ni jukumu lao kuimarisha uhusiano huo mzuri.
“Sisi kizazi cha zamani ni jukumu letu kuhakikisha kuwa tunakieleza kizazi cha sasa kuhusu jitihada za Tanzania katika harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika”
“Tulikuwa tunakuja hapa, jengo hili na Mwalimu Nyerere alikuwa Rais wakati huo, ambapo aliweza kusuluhisha migogoro iliyokuwepo kati ya chama cha ZANU na ZAPU” aliongeza Rais Mnangangwa.
Rais Mnangagwa alisema kuwa serikali yake iko tayari kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali yatakayosaidia kukuza uchumi wake na kuahidi kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu kuisha utaotarajiwa kufanyika Julai 30 mwaka huu, Tume ya Ushirikiano itakutana kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo ya kibiashara.
Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alisema Tanzania na Zimbabwe ni nchi marafiki tangu harakati za uhuru mwaka 1960.
Ambapo mwaka 1982 ilianzishwa Tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya Tanzania na Zimbabwe kupitia taasisi mbalimbli za kimataifa ikiwemo SADC.
Aidha, Rais Magufuli ametaja mikakati ya kukuza na kuimarisha ushirikiano wa uchumi katika maeneo ya sita ambayo ni biashara ambapo nchi hizo zimedhamiria kutumia fursa za SADC za kulegeza masharti ya biashara.
Maeneo mengine ni la kukuza uwekezaji , utalii, usafiri wa anga na barabara, kushirikiana kupitia SADC kwa maana ya fursa za wanachama. Pamoja na eneo la ulinzi, usalama, afya, utamaduni, sanaa na michezo.
Vilevile, Rais Magufuli amesema wanawakaribisha Wazimbabwe kuja kuwekeza nchini Tanzania hasa ukizingatia kwamba kuna kiwango kidogo cha uwekezaji baina ya nchi mbili ambazo ni marafiki wa muda mrefu.
“Mwaka 2006 kiwango cha uwekezaji cha Zimbabwe nchini kilikuwa na thamani ya biashara ya sh. bilioni 18.3, huku mwaka 2017 ikiwa sh. bilioni 21.1, hivyo tumekubaliana kuimarisha baadhi ya maeneo ili kuleta mkakati wa kuimarisha uchumi wa nchi hizi mbili” alisema Rais Magufuli.
Rais Mnangagwa ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, kesho juni 29 anatarajiwa kutembelea Chuo cha Sanaa cha Kaole Bagamoyo ambacho awali kilitumika kutoa mafunzo kwa wapigania uhuru kutoka nchi za Kusini mwa Bara la Afrika. Ambapo Rais Mnangagwa ni miongoni mwa waliopata mafunzo katika chuo hicho.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO