WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameanza ziara fupi ya siku tatu, kukagua miradi ya maendeleo jimboni kwake katika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.
Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, amekagua miradi ya maji, ujenzi wa zahanati na kuzungumza na wananchi katika vijiji vya Mibure, Namakuku, Chienjere, Namahema A na Namahema B.
Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mibure Alhamisi, Desemba 28, 2017 mara baada ya kukagua zahanati ya kijiji hicho, Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na ujenzi unavyoendelea na akamwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ruangwa ahakikishe zahanati hiyo ikikamilika inapata kifaa cha kuwatunzia watoto njiti kwa sababu kijiji hicho kiko mbali na Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa.
“Nilileta makontena yenye vifaa vya hospitali, na humo ndani mlikuwa na vifaa vya kuwatunza watoto njiti (watoto wanaozaliwa kabla ya muda kutimia). Hakikisha hawa wanapata kifaa hicho kwa sababu hawana gari la kubeba wagonjwa, na pia wako mbali na hospitali ya wilaya na pia kituo cha afya cha jirani kiko mbali pia,” alisisitiza.
Akizingumzia kuhusu upatikanaji wa umeme kijiji hapo, Waziri Mkuu alisema: “Mibure ipo kwenye mipango ya kupata umeme ambao unatoka Nagurukuru, -Nghimbwa-Chienjere-Namakuku-Mibure.”
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO