Na: Beatrice Lyimo
Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameihimiza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuharakisha uandaaji wa Sera ya Riba ambayo zitaifanya taasisi za kifedha kuwa na riba zinazowiana na nafuu.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Mjini Dodoma wakati wa akizundua tawi jipya la Benki ya CRDB lililopo jengo la LAPF Makole ambalo ni tawi kubwa kwa mkoa wa Dodoma.
"Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto za mabenki kutolipwa na wakopaji kwa kuanzisha mfumo wa kuhifadhi taarifa za mkopaji ambazo zitawezesha benki zote kuwatambua wakopaji na kuweza kuchukua tahadhari stahiki, pia itaendelea kutoa vitambulishio vya Taifa ambavyo kwa sasa vina taarifa zote muhimu za mwananchi," amefafanua Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli ametoa wito kwa BOT kudhibiti matumizi ya dola na fedha nyingine za kigeni hapa nchini kutokana na kuharibu uchumi wa nchi. Dkt. Magufuli ametolea mfano wa fedha zilizoshikiliwa Airport ya Dar es Salaam ambazo ni zaidi ya Dola Milioni Moja zikiwa hazijulikani zilipokuwa zikipelekwa.
Vile vile ameiagiza BOT kufungia mabenki na makampuni ya simu ambayo hayatajiunga na kituo cha kuhifadhia taarifa ambacho kina mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali kuhakikisha yamejiunga kufikia mwisho wa mwaka vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Rais Magufuli ametoa wito kwa mabenki yote nchini kupeleka huduma za kibenki hadi vijijini kupitia njia mbalimbali kama vile mabenki yanayotembea, mitandao ya simu pamoja na kutumia mawakala ili kuongeza ukwasi kwa mabenki hayo.
Mbali na hayo Dkt. Magufuli ameitaka Benki ya CRDB kuandaa utaratibu wa kujenga Makao Makuu ya Benki hiyo mjini Dodoma kwani Dodoma ndio Makao Makuu ya nchi na tayari Serikali imeshaanza kuhamia.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amewakaribisha wawekezaji mbalimbali kuwekeza katika Mkoa wa Dodoma na kuahidi kutoa ushirikiano kwa wawekezaji hao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei ameipongeza Serikali kwa uamuzi wa ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mifumo ya kielektroniki.
Pia Dkt. Kimei amemkabidhi Rais Magufuli Hundi ya Shilingi Milioni 100 kwa ajili ya ufadhili wa miradi mbalimbali ya kijamii ambapo Rais Magufuli ameikabidhi hundi hiyo kwa uongozi wa Mkoa na kuagiza uongozi huo kujenga Wodi ya wagonjwa katika Hospital ya Mkoa wa Dodoma.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Ali Laay amesema kuwa CRDB imefanikiwa kulipa gawio la shilingi Bilioni 19.5 ambalo lilielekezwa katika uboreshaji wa sekta ya afya nchini.
Mwisho....
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO