Na Dianarose Shirima, MAELEZO
RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amezindua rada za usafiri wa Anga katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICA) na Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro(KIA) ikiwa ni mwendelezo wa mradi uliokuwa umeanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa ajili ya kuhamasisha safari za ndege na kuendeleza Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
Akizungumza katika uzinduzi huo leo Jumatatu (Septemba 16, 2019) Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amewapongeza Wakandarasi wa ujenzi wa mradi huo kutoka nchini Ufaransa kwa kuukamilisha kwa wakati mradi huo kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa mikataba.
Rais Magufuli alisema kuzinduliwa kwa mradi huo kumefungua milango ya ushirikiano na Mataifa ya mbalimbali duniani hususani kuweza kupitisha ndege zao katika anga ya Tanzania kwa kuwa limethibitishia usalama kuwataka wasiogope.
Aidha aliongeza kuwa amesema kuwa licha ya Ndege za ATCL kuanzisha safari ya Mumbai, India serikali imelenga kuanzisha na nchi zingine pia duniani, ikiwemo China na Uingereza na kusisitiza kuwa zingine zitafuata.
Aliongeza kuwa Watanzania hawapaswi kukata tamaa pale zinapotokea changamoto katika harakati za kuleta maendeleo, huku akizungumzia suala la kukamatwa kwa ndege ya Tanzania huko nchini Afrika Kusini ni moja ya changamoto katika maendeleo, hivyo kuwataka Watanzania kuwa na umoja hata pale changamoto zinapotokea bila kuangalia tofauti zao za kisiasa.
Rais Magufuli pia alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Hamza Johari, kutokana na uchapakazi mahiri aliouonesha katika nafasi hiyo, pia akasema kwa mwaka wa fedha uliopita 2018/19, Mamlaka hiyo ilikusanya mapato ya Tsh Billioni 71 kutoka Tsh Billion 40.
Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier, alisema Serikali ya Ufaransa itaendelea kuunga mkono hatua za maendeleo ya uchumi wa Tanzania kupitia viwanda na kusema kuwa Ufaransa ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kuleta maendeleo na kufikia uchumi wa kati kwa maslahi mapana ya taifa la Tanzania ya mataifa hayo.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO