Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Januari, 2020 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 9 walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho ni Mhe. Maria Amelia Maio de Paiva (Balozi wa Ureno hapa nchini), Mhe. Douglas Foo Peow Yong (Balozi wa Singapore hapa nchini), Mhe. Alex Chua (Balozi wa Ufilipino hapa nchini), Mhe. Angela Veronica Comfort (Balozi wa Jamaica hapa nchini) na Mhe. Dkt. Christian Fellner (Balozi wa Austria hapa nchini).
Mabalozi wengine waliowasilisha hati zao za utambulisho ni Mhe. Francisca Ashietey-Odunton (Balozi wa Ghana hapa nchini), Mhe. Jesús Agustin Manzanilla Puppo (Balozi wa Venezuela hapa nchini), Mhe. Yacin Elmi Bouh (Balozi wa Djibouti hapa nchini) na Mhe. Oded Joseph (Balozi wa Israel hapa nchini).
Pamoja na kupokea hati za utambulisho za Mabalozi hao, Mhe. Rais Magufuli amepokea salamu kutoka kwa viongozi wakuu wa nchi hizo ambao wameeleza kufurahishwa kwao na uhusiano na ushirikiano mzuri na Tanzania, na dhamira yao ya kuukuza na kuuendeleza zaidi uhusiano huo.
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi wakuu wa nchi hizo kwa salamu, na amewapongeza na kuwakaribisha Mabalozi walioteuliwa kuziwakilisha nchi hapa nchini.
Amewahakikishia kuwa Tanzania ipo tayari kukuza zaidi uhusiano wake na nchi hizo hasa katika diplomasia ya uchumi, na amewataka Mabalozi hao kuwahamasisha wafanyabiashara kuja kuwekeza hapa Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, madini, mafuta na gesi na biashara nyingine mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili.
Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa anatambua kuwa ushirikiano na nchi hizo utasaidia kubadilishana uzoefu, ujuzi, teknolojia na mitaji itakayosaidia kutumia rasilimali zilizopo Tanzania kwa manufaa ya Watanzania na wananchi wa nchi hizo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Januari, 2020
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO