TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 26 Februari, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Ubongo na Mishipa kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking (PUIH) iliyopo Beijing nchini China Prof. Zhao Yuanil ambaye ameongoza timu ya wataalamu wanaoshirikiana na Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu ya Muhimbili (MOI).
Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Mseru.
Katika mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Hospitali ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking kwa kukubali ombi lake la kuanzisha ushirikiano na MOI na amemhakikishia Prof. Yuanil kuwa Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano zaidi utakaowezesha MOI kuongeza uwezo wake wa kutoa huduma za upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kwa Watanzania ambao wamekuwa wakikosa huduma hiyo ama kulazimika kutumia gharama kubwa kwenda nje ya nchi.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na taarifa za kufanyika kwa mafanikio kwa upasuaji wa kwanza uliofanywa na Daktari Bingwa Prof. Yuanil hapo jana na kwamba anaamini wataalamu zaidi wataendelea kuja hapa nchini kutoka PUIH kwa ajili ya kutoa huduma na kuwafundisha madaktari wa Tanzania, na pia Watanzania wengi watakwenda nchini China kujifunza upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu.
Kwa upande wake Prof. Yuanil amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake kubwa za kuhakikisha MOI inaimarishwa ikiwemo kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu na amemhakikishia kuwa PUIH itahakikisha makubaliano yaliyotiwa saini mwaka jana kati ya hospitali hiyo na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yanatekelezwa kikamilifu.
“Tanzania kuna watu zaidi ya Milioni 50 na kuna idadi kubwa ya watu wenye magonjwa ya ubongo, wanaopata majeraha kichwani, uvimbe wa ubongo, matatizo ya mishipa ya damu ya ubongo na magonjwa ya uti wa mgongo ambao wanahitaji kupata matibabu mazuri hapahapa, lakini naambiwa kuna wataalamu 10 tu ambao hawatoshelezi mahitaji, ndio maana tupo hapa kuangalia mnafanya nini na tuone namna ya kusaidia kuwaongezea uwezo” amesema Prof. Yuanil.
Nae Mhe. Ummy Mwalimu amemshukuruMhe. Rais Magufuli kwa jitihada zake za kuwatafuta Madaktari Bingwa kutoka PUIH na kutoa maelekezo ya kuanzishwa kwa ushirikiano na MOI, pamoja na kuhakikisha Serikali inatoa zaidi ya Shilingi Bilioni 12.5 za kuimarisha miundombinu ya MOI ili itoe matibabu ya kibingwa ya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kwa Watanzania wengi.
“Kwa kweli Watanzania wawe na matumaini makubwa kuwa huduma zile za kibobezi zitapatikana ndani ya nchi na hakuna kwenda nje, mambo yote ndani ya nchi, kwa hiyo tunashukuru sana kwa maono haya ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, yeye ndio alipata taarifa kuwa kuna Daktari Bingwa huyu wa upasuaji wa ubongo na kisha akatupa maelekezo kuwa daktari huyo ameweza kutoa matibabu kwa wagonjwa walioshindikana katika nchi nyingi, kwa hiyo tukafanya mawasiliano kupitia Ubalozi wetu wa China na baadaye tukasaini mkataba Septemba 2018 nilipokwenda China na sasa tumeanza kutekeleza” amesema Mhe. Ummy Mwalimu.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema kupitia ushirikiano huu Tanzania inatarajia kupata wataalamu wengi wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu na amebainisha kuwa pamoja na kufanya upasuaji wa mafanikio kwa mgonjwa mmoja hapo jana, wagonjwa wengine wawili watafanyiwa upasuaji leo na kwamba ushirikiano huu utaiwezesha MOI kuwa kituo bora cha upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu Barani Afrika.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
26 Februari, 2019
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO