RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli Oktoba, 2017 amefungua kiwanda cha kuzalisha bidhaa za plastiki cha Victoria Moulders na kiwanda cha dawa za binadamu cha Prince Pharmaceuticals Co. Ltd vilivyopo katika Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza.
Mmiliki wa kiwanda cha Victoria Moulders Bw.Manjit Singn amemueleza Rais Magufuli kuwa kiwanda hicho pamoja na kiwanda dada cha Poly Bags vilivyopo katika eneo moja la Igogo vimeajiri watu 500 na vinazalisha bidhaa za plastiki ambazo ni Mabomba ya maji, matanki ya maji, ndoo, nyavu na mifuko ya kuhifadhia nafaka.
Kiwanda cha dawa cha Prince Pharmaceuticals kilichopo Buhongwa kinazalisha aina 26 za dawa na uwezo wake ni kuzalisha kilogram 1,400 na lita 5,000 za aina mbalimbali za dawa kwa siku, ambazo husambwazwa kupitia MSD na wafanyabiashara.
Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bw. Hetal Vithlani amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani alipoteza matumaini ya kuendelea na mradi huo lakini sasa amepata matumaini mapya baada ya Serikali kuanza kununua dawa ambapo MSD imeagiza aina 7 za dawa zenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.2 na kwamba ifikapo mwaka 2020 kiwanda kitaongeza uzalishaji wa dawa za maji kutoka lita 5,000 hadi kufikia lita 10,000.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema viwanda hivyo ni muhimu kwa kuwa vipo katika kundi la viwanda vinavyozalisha bidhaa zenye mahitaji makubwa.
Waziri Mwijage amemueleza Rais Magufuli kuwa nchi inahitaji tani Miliomi 15 za mifuko ya kuhifadhia mazao ikilinganishwa na tani milioni 5 zinazozalishwa kwa mwaka hivi sasa, na kwamba juhudi za kuwahamasisha wawekezaji zinaendelea. Kwa dawa za binadamu amesema ndani ya miezi 18 viwanda vitatu vya kutengeneza dawa na kimoja cha kutengeneza dripu za maji ya wagonjwa vitajengwa.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu amesema ujenzi wa viwanda vya dawa utasaidia kuokoa fedha nyingi ambazo Serikali inazitumia kununua dawa kutoka nje ya nchi ambapo hivi asilimia 80 ya dawa zinaagizwa nje ya nchi.
Pamoja na kumshukuru Rais Magufuli kwa msukumo wake wa kuongeza bajeti ya dawa kutoka Shilingi Bilioni 31 hadi kufikia Shilingi Bilioni 269, Waziri Ummy amesema Serikali itajenga kiwanda cha kuzalisha dripu za maji ili kuokoa Shilingi Bilioni 12 ambazo hutumika kila mwaka kuagiza dripukutoka nje ya nchi.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha usambazaji wa dawa na hivi karibuni bodi ya dawa (MSD) itapatiwa magari mapya 190 ya kusambazia dawa nchini na kwamba kutokana na kazi nzuri inayofanywa, MSD imeteuliwa kuwa msambazaji wa dawa katika nchi 15 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Akizungumza baada ya kufungua viwanda hivyo, Rais Magufuli amezipongeza kampuni za Victoria Moulders na Prince Pharmaceuticals kwa kuwekeza viwanda hivyo na ametoa wito kwa wafanyabiashara kote nchini kujitokeza kuwekeza katika ujenzi wa viwanda kwa kuwa Serikali itawaunga mkono.
“Niwaombe wafanyabiashara wa Tanzania na wasomi, badala ya kulalamika fedha zimepotea jengeni viwanda, huyu mwenye kiwanda cha Prince Pharmaceuticals alikuwa anataka kufunga mradi wa kiwanda hiki lakini baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani anapata fedha, haingii akilini nchi iwe inaagiza dripu kutoka nje ya nchi” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli ametoa wiki mbili kwa wawekezaji waliopewa viwanda vya TPI na Keko Pharmaceuticals ambavyo Serikali ina hisa, kuanza uzalishaji mara moja vinginevyo wanyang’anywe na wapewe wawekezaji ambao wapo tayari kuanza uzalishaji.
“Mhe. Waziri umewapa mwezi mmoja ni muda mrefu mno, mimi nawapa wiki mbili wawe wameanza uzalishaji wa dawa, tumewasubiri imetosha, kama hawawezi kuanza kutengeneza dawa wapewe wengine wenye uwezo” amesisitiza Rais Magufuli.
Akiwa njiani wakati wa kutembelea viwanda hivyo, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Butimba na kuwahakikishia kuwa Serikali imedhamiria kurejesha viwanda vilivyokuwepo kati ya eneo la Mkuyuni na Igogo Mjini Mwanza kikiwemo kiwanda cha kusaga nafaka ambacho Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) tayari limetenga Shilingi Bilioni 8 kwa ajili ya kukifufua.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO